Uandishi | Kiswahili Kidato cha Pili

 

Bahasha ya kaki.

Insha za hoja

Insha za hoja ni insha zinazoelezea jambo fulani katika hali ya kujenga hoja ambazo zinatetea msimamo fulani alionao mwandishi wa insha hiyo juu ya jambo analolizungumzia. Hoja ni maelezo bayana yanayotolewa na mwandishi kutetea msimamo wake.
Katika uandishi wa insha za aina hii, mwandishi hutakiwa kuonesha ni jambo gani ambalo analiunga mkono na ni lipi ambalo hakubaliani nalo.
Ili hoja zote zipate kueleweka ni sharti zipangwe katika mtiririko wa mawazo ulio sahihi kiasi kwamba mtu aisomapo anapata kuelewa ni mada gani mwandishi anaijadili na ana msimamo gani kuhusu mada hiyo.

Mambo ya Kuzingatia Katika Uandishi wa Insha za Hoja

Unapoandika insha za hoja, au aina zingine za insha, zingatia mambo haya:
1. Kubaini mada ya kuandikia insha na kuielewa vyema.
2. Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki.
3. Kutumia mtindo unaoendana na kusudi la insha. Kwa mfano, mtindo wa masimulizi, unafaa kwa hadithi au insha zingine za kisanaa.
4. Kutumia lugha fasaha na inayoeleweka.
5. Kufuata kanuni za uandishi. Kwa mfano, matumizi ya alama za uandishi, aya, herufi kubwa na ndogo, n.k
6. Kupanga insha katika muundo wake, yaani kichwautangulizikiini na hitimisho.

Mfano wa Insha ya Hoja

VIJANA NA STAREHE
Vijana wengi, wake kwa waume, wamekuwa wakijiingiza katika starehe zisizofaa ikiwemo, utumiaji wa madawa ya kulevya kama: pombe, unga na bangi. Vijana hawafanyi kazi kwa kuelemewa na starehe. Jambo hili siyo zuri na linaweza kuleta maafa makubwa.
Vijana hawa watakuwa na mwisho mbaya kwani pombe na vilevi vingine wanavyotumia vinaharibu afya zao na hivyo kufupisha maisha na kuwapa mzigo wanaowategemea pindi watakapoanza kuwauguza.
Vijana hawa hawatakuwa na maendeleo yoyote na endapo watafika uzeeni hawatakuwa na kitu kwa sababu nguvu zao za ujana walizitumia katika mambo yasiyofaa.
Mbali na hayo, vijana hawa wanakabiliwa na hatari ya kuugua magonjwa ya kuambukiza kwa sababu wawapo katika starehe, wamekuwa wakijihusisha na tabia hatarishi.
Endapo vijana hawatazinduka na kuacha starehe, watakabiliwa na mwisho mbaya ambao utazidi kufanya nchi yetu iendelee kuwa masikini.

Barua Rasmi

Barua rasmi ni barua zinazohusu mambo rasmi ya kiofisi.

Dhima za barua rasmi

Dhima za barua rasmi ni:
1.   kutoa taarifa.
2.   kuomba kazi au huduma.
3.   kuagiza vitu na kutoa mwaliko kwa mfano kwa kiongozi fulani wa nchi.
4.   kutoa malalamiko na kuweka kumbukumbu au marejeo.

Mfano wa barua rasmi

Mtaa wa Kisutu,
S.L.P 25,
Kinondoni Dar es Salaam.
28/01/2019.
Mkuu wa shule,
Shule ya Sekondari Kigoma,
S.L.P 175,
Kigoma.
Ndugu,
Yah: KUTUMIWA CHETI
Husika na kichwa cha barua hapo juu. Nilihitimu kidato cha nne katika shule yako mwaka 2011. Kwa muda wote huo, sikuweza kuchukua cheti changu cha kuhitimu elimu ya kidato cha nne.
Ninaomba unitumie cheti hicho kwa njia ya posta na nitashukuru sana endapo utafanya hivyo.
Wako mtiifu,
A. Maiga
Chacha Maiga

Simu ya maandishi

Simu ya maandishi ni aina ya barua fupi ambazo husafirishwa kwa haraka sana kuliko barua za kawaida.
Simu hizo huandikwa kwenye fomu maalumu ambazo hutolewa na shirika la posta. Simu za maandishi hujulikana kama telegram.
Gharama za simu za maandishi hutozwa kulingana na idadi ya maneno yaliyotumika. Kwa hiyo ujumbe unaotumwa huandikwa kwa maneno machache ili kuepuka kutozwa gharama kubwa.
Dhima ya simu ya maandishi ni kutuma ujumbe wa dharura. Hivyo simu ya maandishi huandikwa kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa haraka.

Mfano wa simu ya maandishi:

ABELI MATHIAS SLP 5299 DSM NJOO HARAKA DADA MGONJWA SINGIDA

Kadi za mialiko

Kadi za mialiko ni aina ya karatasi ngumu zinazopeleka taarifa fupi za kumwomba mtu ahudhurie katika sherehe fulani kama vile harusi, ubatizo mahafali n.k

Mfano wa Kadi ya Mwaliko

Kadi ya Mwaliko

Uandishi wa dayolojia

Dayalojia ni mazungumzo au majibizano baina ya watu wawili au zaidi wanaozungumza kwa kupokezana. Kama zilivyo kazi nyingine za utungaji, dayalojia inaweza kuwasilishwa kwa nijia ya mazungumzo au maandishi.

Mfano wa dayalojia

KIMATI:    (Anaonekana mwenye furaha,anamwita rafiki yake, Tazaa) Wow, Tazaa! Tumekutana tena, nafurahi kukuona! (wanakumbatiana wote wakitabasamu.)
TAZAA:      (Anatabasamu huku ameshikilia mkono wa kulia wa Kimati, anaonesha shauku kuu.) Kimati! Bado unanikumbuka? Nina furaha sana kwa kweli, ni muda mrefu sana.
KIMATI:     (Anachekelea) Aaaah, nahisi kama naota Tazaa, siamini kama nimekutana na wee leo hii ni muda mrefu sana, nimefurahi kwa kweli.
TAZAA:      (Anachekelea).
KIMATI:     Mbona wachekelea tu…. Sema jambo rafiki.

Maswali

1.   Eleza namna barua rasmi zinavyotofautiana na barua za kirafiki.
2.   Tunga dayolojia kuhusu athari za madawa ya kulevya

Comments

Popular posts from this blog

Usimulizi | Kiswahili Kidato cha Pili

Matumizi ya Lugha Katika Miktadha Mbalimbali