Usimulizi | Kiswahili Kidato cha Pili
Usimulizi ni jumla ya maelezo yanayotolewa na mtu au watu wengi kuhusu tukio fulani. Tukio hilo linaweza kutokea katika wakati mfupi uliopita au zamani kidogo.
TUKIO LA MZEE NA KONDAKTA
Jana nikiwa nimepanda daladala, kulitokea tukio la Mzee na kondakta wa daladala. Tukio hili lilitoka muda wa saa sita mchana.
Kondakta alimfuata Mzee na kumwomba ampe nauli, Yule mzee alidai kuwa, nauli alilipa. Kondakta alidai kama mzee amelipa basi aoneshe tikiti yake. Mzee alidai kuwa, alipotoa fedha, hakupewa tikiti. Pia, mzee alitetewa na watu wengi ambao walidai walishuhudia akilipa nauli. Hata hivyo, kondakta alibaki katika msimamo wake uleule wa kumtaka Mzee alipe nauli au aonyeshe tikiti.
Baada ya usumbufu kuwa mkubwa, mzee alisimama akakunja ngumi, konda naye akakunja. Mzee akarusha ngumi nzito, loooh! Konda alianguka mpaka chini.
Dereva alikuja kusaidia, hata hivyo Mzee alikuwa imara, dereva alipigwa ngumi ya kichwa akadondoka hatua mbili alipodondoka konda.
Dereva na konda walilala chini walioumizwa na zile ngumi za Mzee. Watu walimshangilia na kumpongeza. Mwisho, dereva aliinuka, konda akafuatia, gari ikawashwa na kuendelea na safari.
Taratibu za usimulizi wa matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Maswali
1. Taja mbinu muhimu za usimulizi wa habari.
2. Ni upi umuhimu wa usimulizi wa habari katika maisha yetu ya kila siku.
3. Endeleza usimulizi huu kwa maneno yasiyozidi ukurasa mmoja.
Comments
Post a Comment