Ufahamu

 Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.

Ufahamu wa Kusikiliza

Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.

Kujibu Maswali ya Ufahamu kutokana na Habari uliyoisikiliza

Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:

  • Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
  • Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza
  • Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa.

Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:

  1. Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.
  2. Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.
  3. Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
  4. Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.

Kufupisha kwa Mdomo Habari uliyoisikiliza

Ili kuweza kufupisha kwa mdomo habari uliyoisikiliza yapo mambo ya kuzingatia. Mambo hayo ni kubaini mawazo makuu yanayopaswa yajitokeze katika habari iliyofupishwa, kupanga maelezo kwa usahihi katika usemaji, kuzingatia kichwa cha habari ambacho kinapaswa kihusiane na ufupisho na wazo kuu na mwisho ni kusema ufupisho kwa ufasaha na kwa lugha ambayo ni nzuri.

Ufahamu wa Kusoma

Ufahamu wa kusoma ni ule mtu anaoupata kwa njia ya kusoma makala, kifungu cha habari, kitabu au gazeti.

Kusoma kwa Sauti kwa kuzingatia Lafudhi ya Kiswahili

Kuna vipengele viwili vinavyounda mchakato wa ufahamu wa kusoma:

  • Uelewa wa msamiati na
  • Uelewa wa matini

Ili kuilelewa habari/matini ni lazima msomaji awe na uwezo wa kuelewa msamiati uliotumika katika matini hiyo. Endapo maneno yaliyotumika hayataeleweka vilevile matini yote hataeleweka.

Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:

  1. Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je, kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
  2. Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi kama mkato, nukta, nukta-mkato, n.k., kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
  3. Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
  4. Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.

Kwa kuzingatia haya yote msomaji atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha habari hiyo aliyoisoma.

Kujibu Maswali kutokana na Habari uliyoisoma

Ili kujibu maswali yanayotokana na habari uliyoisoma inatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo; kubaini mawazo makuu, kuzingatia alama za uandishi, kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali na kutilia maanani vidokezo vya maana. Aidha mawazo yanapaswa kuelekezwa katika jambo linalosomwa, kujiuliza maswali kadri unavyosoma na kuandika ufupisho.

Kufupisha Habari uliyoisoma

Ili kuandika ufupisho mzuri wa habari uliyosoma yapaswa kuzingatia yafuatayo: kuisoma habari uliyopewa zaidi ya mara moja, kubainisha mawazo makuu, kuandika ufupisho kwa lugha fasaha na yenye mtirirko mzuri wa hoja, kuhesabu idadi ya maneno na kuhakikisha haizidi idadi inayotakiwa na kupitia habari ya mwanzo na kisha ufupisho ili kuona kama taarifa muhimu haijaachwa au kusahaulika.

Kusoma kwa Burudani

Huu ni usomaji ambao lengo lake kuu huwa ni kujiburudisha tu. Katika usomaji wa aina hii, msomaji hujisomea zaidi magazeti, majarida na vitabu tofauti na vile vinavyotumika darasani.

Wakati mwingine sio lazima msomaji awe na vitabu vyote ambavyo anahitaji kuvisoma au magazeti na majarida. Inapotokea hivyo, msomaji anaweza kwenda maktaba kuazima kitabu nachokihitaji.

Ingawa lengo la msomaji huwa ni kujiburudisha tu, lakini pia hujiongezea maarifa. Hii ni kwa sababu, magazeti, majarida na vitabu sambamba na kutumia lugha sanifu huelezea mambo mabalimbali yanayoihusu jamii.

Mambo ya Kuzingatia katika Ufahamu wa Kusikiliza

Msomaji kutokana na kusoma vitabu na majarida mbalimbali hujiongezea kiwango cha welewa wa lugha na mambo mengine ya kijamii yanayojadiliwa humo.

Ni jambo zuri kwa msomaji kujijengea tabia ya kujipima ili aweze kuelewa kiwango cha maarifa aliyopata katika kujisomea. Kujipima huku kunaweza kufanywa kwa kujiundia utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya vitu au makala zilizosomwa na kufanya ufupisho wa kila makala.

Utaratibu unaopendekezwa katika kujipima na kujiwekea kumbukumbu ya usomaji wa burudani ni kama ufuatao:

  1. Tarehe…
  2. Jina la kitabu/makala/gazeti….
  3. Mchapishaji……
  4. Mwaka/tarehe ya uchapishaji…..
  5. Ufupisho wa habari(yasizidi maneno 20)
  6. Fundisho/ujumbe mkuu ni…..
  7. Jambo lililokuvutia sana……
  8. Maoni kwa ujumla kama yapo….

Matumizi ya Kamusi

Kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa. Au kamusi ni orodha ya maneno yaliyo katika karatasi au nakala tepe yaliyopangwa kialfabeti na kutolewa maana pamoja na maelezo mengine na kuhifadhiwa katika kitabu, santuri, simu, tarakilishi au katika mfumo wowote wa kielekroniki.

Jinsi ya Kutumia Kamusi

Maneno yanayoingizwa katika kamusi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufi a, yote huwekwa chini ya herufi A. Maneno yanayoanza na herufi fulani nayo hupangwa katika utaratibu wa alfabeti kwa kuzingatia herufi ya pili, ya tatu, nne au tano ya neno kama mfano hapa chini unavyoonyesha.

Mfano:ja, jabali, jabiri, jadhibika, jadi.

Maneno yote yanaanza na herufi [j]. herufi ya pili kwa maneno yote ni [a]. herufi ya tatu ni [b] na [d]. Kwa kuwa [b] hutangulia [d] katika mpangilio wa alfabeti maneno yenye [b] kabla ya yale yenye [d]. Kwa kuwa maneno yenye herufi [b] ni mawili itabidi tutazame herufi ya nne ya hya maneno ili tuchague litakaloorodheshwa mwanzo. Neno ‘jabali’ litaorodhewshwa kabla ya ‘jabiri’ kwa kuwa [a] (herufi ya nne) ya ‘jabali’ hutangulia [i] ya ‘jabiri’ ambayo pia ni herufi ya nne. Kisha tunatazama maneno yenye [d] kama herufi ya tatu. Hapa tunaangalia pia herufi ya nne ili kubaini neno litakaloandikwa mwanzo kati ya ‘jadhibika’ na ‘jadi’. Kwa kuwa [h] hutangulia [i] basi ‘jadhibika’ huorodheshwa mwanzo ndipo lifuatiwe na ‘jadi’.

Kwa hiyo hivi ndivyo unavyopaswa kutafuta neno kwenye kamusi. Nenda kwenye herufi ya neno ulalotafuta alafu litafute kwa kufuata mlolongo huo huo wa herufi ya kwanza kuorodheshwa.

Neno linaloorodheshwa kwenye kamusi ili lifafanuliwe linaitwa kidahizo.Kidahizo huandikiwa maelezo ya kukifafanua. Maelezo haya ni matamshi ya kidahizo, maana ya kidahizo, kategoria ya kisarufi, sentensi ya mfano wa matumizi ya kidahizo n.k. Kidahizo pamoja na maelezo yake ndio huitwa kitomeo cha kamusi.

Kutafuta maana unayoitaka

Neno linaweza kuwa na maana moja au zaidi ya moja. Maana inapokuwa moja mtumiaji kamusi hana tatizo kwani hiyo ndiyo atakayoipata na kuichukua. Lakini neno linapokuwa na maana zaidi ya moja, mtumiaji kamusi hutatizika asijue ni ipi aichague. Ili kupata maana inayosadifu itafaa mtumiaji kamusi kutafuta maana ambayo inahusiana na muktadha wa neno linalotafutwa.

Example 1

Mfano:kifungo nm vi-

  • kitu cha kufungia
  • kitu kinachotumiwa kufungia vazi kama vile shati, gauni, suruali n.k
  • adhabu ya mtu kuwekwa jela kwa muda fulani

Iwapo mtumiaji aliona neno ‘kifungo’ kwa muktadha wa: “Juma alihukumiwa kifungo cha miaka kumi baada ya kupatikana na hatia ya kubaka….” Maana ya mukatadha huu itakuwa ni ile maana ya 3 kwa sababu ndiyo yenye kuhusiana na muktadha ambapo neno kifungo limetumika na wala sio maana ya 1 wala ya 2.

Comments

Popular posts from this blog

Usimulizi | Kiswahili Kidato cha Pili

Uandishi | Kiswahili Kidato cha Pili

Matumizi ya Lugha Katika Miktadha Mbalimbali